WAZIRI NDALICHAKO ASISITIZA USIMAMIZI WA MTAALA SEKTA YA ELIMU MSINGI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesisitiza Maafisa Elimu Mikoa, Wilaya na Maafisa Elimu Taaluma Mikoa kuhakikisha wanaimarisha usimamizi wa Mtaala unaotumika kufundishia Elimu Msingi Nchini ili kukidhi mahitaji.
Mhe. Waziri Ndalichako ameyasema hayo Juni 03, 2021 Mjini Bagamoyo wakati akifungua mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani kwa Maafisa Elimu Mikoa, Wilaya na Maafisa Elimu Taaluma Mikoa yanayoendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) katika Kampasi yake ya Bagamoyo yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa namna bora ya kusimamia Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani katika maeneo yao.
“Ubora wa Mtaala, unaendana na Usimamizi, nendeni mkasimamie vizuri mtaala unaotumika sasa kufundishia elimu ya Msingi Nchini, fanyeni ufuatiliaji wa namna walimu wanafundisha mashuleni, angalieni kama wanafundisha kwa kufuata mtaala wetu ili kukidhi mahitaji ya ufundishaji na ujifunzaji yatakayotoa wahitimu wenye maarifa na ujuzi wa kutosha” Amesema Profesa Ndalichako
Amesema mafunzo ya Uthibiti Ubora wa Shule wa Ndani waliyopatiwa, yawe chachu ya ya kwenda kufanya mabadiliko katika Sekta ya Elimu Msingi Nchini kwa kuhakikisha yanawasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi kwa kujifunza kutoa takwimu sahihi na za kweli zinazohusiana na Sekta ya elimu ili Wizara ijue namna bora ya kutatua changamoto za Kisekta katika maeneo yao na kuacha tabia ya kutoa takwimu za uongo kwa kuogopa kuonekana wameshindwa kutekeleza majukumu yao.
Waziri Ndalichako pia amesisitiza usimamizi mzuri katika Fedha za uboreshaji wa Miundo mbinu ya elimu zinazotumwa katika kila Halmashauri na kuwataka Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati, ili lengo la Serikali la kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji liweze kufikiwa.