ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

ADEM YASHIRIKI UZINDUZI WA MPANGO WA USHIRIKIANO KATI YA TAASISI ZA ELIMU NA VIWANDA

12 Feb, 2026
ADEM YASHIRIKI UZINDUZI WA MPANGO WA USHIRIKIANO KATI YA TAASISI ZA ELIMU NA VIWANDA

Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri wa Kitaalamu na Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala wakiwa pamoja na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Ushauri Dkt. Coretha Komba na Dkt. Richard Kayombo wamehudhuria kwenye uzinduzi wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu -Vyuo Vikuu, Vyuo vya Kati, Vyuo vya Ufundi na Viwanda unaofanyika leo Februari 9, 2026 katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.

 

Uzinduzi huo ni muendelezo wa mageuzi ya elimu yanayolenga kutafuta mwafaka na kujadili ni kwa namna  gani Vyuo Vikuu, Vyuo vya Kati na Taasisi zingine za Elimu zinazotoa mafunzo ya nadharia watashirikiana na viwanda ili wanafunzi wapate fursa ya kujifunza kwa kutumia vifaa vya kisasa katika viwanda mbalimbali nchini kwani vyuo vingi havina mazingira hayo wezeshi ya vifaa vya kisasa vinavyotakiwa kuwaandaa na kuwajengea uwezo wanafunzi kwa mafunzo ya vitendo.

 

Mpango huu utawezesha kupata wahitimu watakaokuwa na ujuzi tayari kushiriki katika uchumi wa viwanda pamoja na kuwaandaa wahitimu kuondokana na wazo la kuajiriwa badala yake wajipatie utalaamu wa kuweza kujiajiri katika sekta binafsi nchini.

 

Mpango huu unachagiza ushirikiano kati ya Serikali na sekta ya Viwanda ukionesha kuwa elimu si jukumu la Serikali pekee, bali ni jukumu la jamii nzima.