HISTORIA YA ADEM
Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu - ADEM ni Wakala wa Serikali ulioanzishwa chini ya Sheria ya Wakala za Serikali (Executive Agencies Act), Sura ya 245. ADEM ina jukumu la kuisaidia Serikali kupitia Wizara zinazosimamia elimu kwa maana ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuhakikisha uboreshaji wa usimamizi wa elimu nchini kupitia utoaji wa mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa elimu, kufanya tafiti mbalimbali na kutoa huduma za ushauri elekezi, pia kuandaa na kuchapisha moduli na vitabu vinavyohusu namna bora ya kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu nchini.
Kuanzishwa kwa Wakala huu kunakwenda sambamba na jitihada za Serikali katika kutekeleza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu.
Ili kutekeleza Dira ya 2050, sekta ya elimu inahitaji rasilimali watu wenye ujuzi na maarifa ya kusimamia na kuendesha taasisi mbalimbali, ikiwemo taasisi za elimu. ADEM inatekeleza majukumu yake kupitia Kampasi tatu zilizopo Bagamoyo, Mwanza na Mbeya.
Makao Makuu ya ADEM yapo katika Mji wa Bagamoyo, umbali wa kilomita 66 Kaskazini Mashariki mwa Jiji la Dar es Salaam. Kampasi ya ADEM–Mwanza ipo katika Jiji la Mwanza, ndani ya Rock City Mall, Jengo C, Ghorofa ya Pili, wakati Kampasi ya ADEM–Mbeya ipo katika Jiji la Mbeya, eneo la Iwambi.
Awali, ADEM ilijulikana kama Taasisi ya Mafunzo ya Usimamizi wa Watumishi wa Elimu (Management Training of Educational Personnel – MANTEP) iliyoanzishwa mwaka 1978. Taasisi ya MANTEP ya zamani na baadaye ADEM zimekabidhiwa jukumu la kutoa mafunzo kwa watumishi wa elimu wakiwemo walimu, wakuu wa shule, maafisa elimu, maafisa uthibiti ubora wa shule, kamati za shule, bodi za shule pamoja na wamiliki na wasimamizi wa shule katika nyanja za uongozi wa elimu, usimamizi wa elimu na uthibiti ubora wa shule, kupitia programu za mafunzo ya muda mfupi na ya muda mrefu.
Kwa sasa, programu za muda mrefu zinazotolewa ni pamoja na Stashahada ya Uongozi, Usimamizi na Utawala wa Elimu (DELMA) ya miaka miwili na Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule (DSQA) ya miaka miwili.
