WALIMU WAKUU ZINGATIENI MISINGI YA UTAWALA BORA ILI KUIMARISHA UONGOZI SHULENI: PROF. NOMBO
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo Oktoba 2, 2023 alipokuwa akifungua mafunzo ya Uongozi, Usimamizi na Uendesha wa Shule yanayotolewa kwa Walimu Wakuu wa Mkoa wa Pwani na Dar Es Salaam, katika kituo cha ADEM Bagamoyo kwa muda wa siku tatu.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo Prof. Nombo amebainisha kuwa Utawala Bora katika Elimu ni injini ya kuimarisha elimumsingi nchini hivyo Walimu wakuu wana wajibu wa kuhakikisha wanazingatia misingi ya Utawala Bora wa Elimu wanapokua katika Utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Prof. Nombo amebainisha kuwa mafunzo hayo ya Uongozi, Usimamizi na Uendesha wa Shule ambayo yatawasaidia Walimu Wakuu kuifahamu misingi ya Utawala Bora wa Elimu yanaendelea sasa katika Mikoa Mara, Pwani, Dar Es Salaam, Morogoro, Dodoma, Songwe na Njombe katika awamu ya kwanza huku lengo likiwa ni kuwafikia Walimu Wakuu wote 17,897 nchini.
“Naipongeza sana Menejimenti ya ADEM kwa kuandaa mafunzo haya, ni imani yangu yameratibiwa vizuri na yatasimamiwa na kuendeshwa kwa weledi na umahiri mkubwa ili yalete tija inayotarajiwa na Serikali”. Amesema Prof. Nombo.
Ameongeza kuwa, mbinu shirikishi zitumike zaidi katika kuwezesha mafunzo hayo ili iwe rahisi kueleweka kwa washiriki na kuwataka washiriki kuwa wadadisi, kuwa huru katika kuchangia maoni yao ili waweze kujifunza kwa ufanisi zaidi kupitia mafunzo hayo.
Prof. Nombo amebainisha kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa mradi wa BOOST kupitia afua namba 8, inayolenga kuimarisha Utawala Bora wa Elimu katika ngazi ya Shule na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kupitia mafunzio hayo Walimu Wakuu wote nchini watajengewa umahiri wa kusimamia vizuri shughuli za Uendeshaji wa Shule na Afua zingine za mradi, ambazo ni kuboresha miundombinu ya elimu, kuimarisha usalama Shuleni, kuongeza uandikishaji wa wanafunzi, kuimarisha elimu ya awali, kuimarisha jumuiya za kujifunza kwa walimu-MEWAKA, kuimarisha vituo vya walimu wanavyotumia kujiendeleza na matumizi ya TEHAMA huku akiwataka washiriki kwenda kuyatumia katika kusimamia afua hizo kwenye mradi wa BOOST.
“Nawaomba mwende mkazingatie misingi ya Utawala Bora katika uendeshaji wa Shule, Uadilifu katika usimamizi wa miradi yote inayotekelezwa Shuleni, kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo ya Manunuzi ya Umma, Ustawi na Usalama wa wanafunzi Shuleni, Usimamizi wa Rasilimali za Shule kwa uadilifu, Ufundishaji na Ujifunzaji kwa ufanisi, Ushirikishwaji wa jamii katika utatuzi wa migogoro na kushughulikia malalamiko Shuleni kwa wakati, matumizi mazuri ya fedha na matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi na upangaji wa mipango mbalimbali ya Shule, na haya yote mtafundishwa kupitia mafunzo hay ana tutakuja kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wake baada ya kukamilika kwa mafunzo”. Amesema Prof. Nombo.
Mtendaji Mkuu ADEM, Dkt. Siston Masanja Mgullah akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo amesema ADEM imejipanga kwa kuandaa Timu ya wawezeshaji mahiri kuendesha mafunzo hayo kwa weledi ili yawe na tija na malengo ya Serikali yafikiwe.
“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Benki ya Dunia kupitia programu ya BOOST kwa kuimini ADEM kuratibu, kusimamia na kuendesha mafunzo haya kwa Walimu Wakuu nchini, na tunaahidi kutekeleza kazi hii kwa weledi na umahiri mkubwa ili kufikia adhma ya Serikali ya kuwajengea uwezo Walimu Wakuu kuhusu Uongozi, Usimamizin a Uendeshaji Fanisi wa Shule” Amesema Dkt. Masanja.
Dkt. Masanja ametumia fursa hiyo kuomba mafunzo hayo pia yaendeshwe kwa Wakuu wa Shule za Sekondari, kwani na wao wana changamoto zinazofanana na za walimu wakuu wa shule za Msingi katika eneo la Uongozi, Usimamizin a Uendeshaji wa Shule, pia kwa Maafisa Elimu Kata, Maafisa Elimu ngazi ya Halmashauri, Mkoa na Wathibiti Ubora wa Shule na wapewe mafunzo haya ili waweze kusaidia walimu wakuu pale wanapokwama.
Ameongeza kuwa kwa sasa mafunzo hayo yameshatolewa kwa Maafisa Elimu Taaluma ngazi ya Halmashauri ili wawe rejea pale ambapo walimu wakuu watahitaji msaada kutoka kwao katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Mafunzo yoyote yanayotolewa hulenga kutoa maarifa, ujuzi na kubadili mtazamo kuwa chanya, mafunzo haya pia yamelenga kujenga umahiri kuhusu Uongozi, Usimamizi, na Uendeshaji fanisi wa Shule mnazosimamia na yatakapokamilika kila mmoja ajiulize amepata maarifa, ujuzi na yamemsaidia kubadili mtazamo wake katika utekelezaji wa majukumu yake? hapo tutakuwa tumefikia lengo la utoaji wa mafunzo haya. Amesisitiza Dkt. Masanja.
Aidha, Dkt. Masanja amesema Walimu Wakuu hao wanajengewa uwezo katika maeneo ya Uongozi, Usimamizi na Utawala Bora wa Shule, Utawala Bora katika elimu, Uendeshaji wa ofisi ya Mwalimu Mkuu, Utunzaji wa kumbukumbu shuleni, Ukusanyaji wa takwimu na uandaaji wa Mpango wa Jumla wa Maendeleo ya Shule, Motisha kwa wafanyakazi, Usimamizi wa Ufundishaji na Ujifunzaji kwa ufanisi shuleni, Usimamizi wa rasilimali vitu shuleni, Ustawi na usalama wa wanafunzi shuleni, Ufuatiliaji na usimamizi wa ufanisi wa shule, Usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya shule na Ushirikishwaji wa jamii katika utatuzi wa malalamiko katika elimu
Bi. Rehema Ramole mshiriki wa mafunzo na Mwenyekiti wa Umoja wa Walimu Wakuu nchini-TAPSHA akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake ameishukuru Serikali kupitia mradi wa BOOST kwa kuona umuhimu wa Walimu Wakuu kupatiwa mafunzo hayo na kwamba wapo tayari kujifunza na kwenda kuyafanyia kazi yale watakayojifunza kwa weledi ili kufanikisha adhma ya Serikali kuendesha mafunzo hayo.