ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

ADEM YAENDESHA MAFUNZO YA UONGOZI NA USIMAMIZI WA SHULE KWA WAKUU WA SHULE NA MAAFISA ELIMU KATA MKOANI MTWARA

07 Dec, 2022
ADEM YAENDESHA MAFUNZO YA UONGOZI NA USIMAMIZI WA SHULE KWA WAKUU WA SHULE NA MAAFISA ELIMU KATA MKOANI MTWARA

Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari pamoja na Maafisa Elimu Kata 228 wameanza kupatiwa mafunzo maalum ya Uongozi na Usimamizi wa Shule yanayotolewa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Mkoani Mtwara.

Mafunzo hayo yameanza rasmi Disemba 05, 2022 na yatakamilika Disemba 22, 2022 ambapo yatafanyika katika Kanda tatu, ambazo ni Kanda ya Masasi itakayojumuisha Halmashauri za Masasi Mji, Masasi (V) na Nanyumbu, Kanda ya Newala itakayojumuisha Halmashauri za Newala Mji, Newala (V) na Tandahimba, Kanda ya Mtwara itakayojumuisha Halmashauri za Mtwara Manispaa, Mtwara (V) na Nanyamba Mji. Aidha, katika kila Kanda mafunzo hayo yatafanyika kwa siku sita, huku katika awamu hii ya kwanza Wakuu wa Shule na Maafisa Elimuj Kata 228 kutoka Halmashauri za Masasi Mji, Masasi Vijijini na Nanyumbu.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo uliofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Wasichana Masasi, Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe Claudia Kitta amesema Mkoa wa Mtwara unakabiliwa na Changamoto za Kata kushindwa kusimamia Ufundishaji, Ujifunzaji na Upimaji, baadhi ya walimu kushindwa kutumia Mbinu Shirikishi, Viongozi wa Elimu kushindwa kutafsiri na kutekeleza Sheria, Kanuni na Taratibu za Uendeshaji wa Shule za Msingi na Sekondari, Wakuu wa Shule na Maafisa Elimu Kata kutozisimamia ipasavyo Timu za ndani za Uthibiti Ubora wa Shule, Ufuatiliaji dhaifu wa Ufundishaji katika Madarasa ya Awali, Darasa la kwanza na Darasa la pili.

“Changamoto hizi ndizo zimesababisha uongozi wa Mkoa kuona upo ulazima kwa viongozi wa elimu katika ngazi husika kupata mafunzo, tunahitaji viongozi mahiri na wanaojitambua katika kutekeleza mikakati hiyo na hivyo kuleta maendeleo katika elimu ndani ya Mkoa wa Mtwara” Amesema Mhe Kitta

Ameongeza kuwa, Elimu ndiyo silaha muhimu ya kupambana na ujinga, maradhi na umaskini ikiwa ni pamoja na kuwa na watu wenye maarifa, ujuzi uzalendo na uaminifu wa kutosha wa kupambana na changamoto za elimu ndani ya Mkoa hivyo kila mwalimu ajitafakari binafsi ili aweze kuchukua hatua ya kuwa mzalendo na mahiri katika kufanikisha azma hii ya Serikali ya kuboresha Elimu kwa wanafunzi anaowafundisha.

“Nitoe wito kwa washiriki wa mafunzo haya kuwa wasikivu na wadadisi katika kipindi chote cha mafunzo ili malengo ya mafunzo yaweze kufikiwa kwani matarajio yetu baada ya mafunzo haya ni washiriki wote warudi katika maeneo yao na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili kwa weledi mkubwa” Amesisitiza Mhe Kitta.

Nae Naibu Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Alphonce Amuli akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo amesema, Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule yanaendeshwa na ADEM katika Mkoa wa Mtwara yanafanyika baada ya Ufuatiliaji uliofanywa na Uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na wadau wengine wa Elimu kubaini mapungufu kwa Viongozi wa Elimu.  Hivyo ADEM imejipanga kuendesha Mafunzo hayo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Wakuu wa Shule na Maafisa Elimu kata Mkoani Mtwara kwa kuzingatia changamoto halisi zinazokabili uendeshaji na usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji katika Mkoa wa Mtwara na yatalenga kuwajengea Umahiri Viongozi hao wa Elimu katika nyanja ya Ufundishaji na Ujifunzaji.