ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

PROF. NOMBO AZINDUA MPANGO WA MAFUNZO YA UONGOZI NA USIMAMIZI WA ELIMU KWA WAKUU WA SHULE ZA SEKONDARI NCHINI

03 Jun, 2026
PROF. NOMBO AZINDUA MPANGO WA MAFUNZO YA UONGOZI NA USIMAMIZI WA ELIMU KWA WAKUU WA SHULE ZA SEKONDARI NCHINI

MWANZA: SERIKALI imezindua rasmi Mpango wa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu kwa Wakuu wa Shule za Sekondari na Maofisa Elimu Kata nchini, hatua inayolenga kuimarisha ufanisi wa uongozi wa shule, usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji na kuimarisha ubora wa elimu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo leo Mei 28, 2026 mkoani Mwanza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema mpango huo ni hatua muhimu katika kujenga uwezo wa viongozi wa elimu hususan wakuu wa shule za sekondari ambao kwa muda mrefu hawajapata mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu kwa kiwango kinacholingana na mahitaji ya sasa ya mfumo wa elimu.

Amesema tofauti na walimu wakuu wa shule za msingi ambao wamekuwa wakipata mafunzo ya uongozi, wakuu wa shule za sekondari wamekuwa wakikosa fursa hiyo kwa kipindi kirefu, hali iliyofanya Serikali kuona umuhimu wa kuanzisha mpango huo wa kitaifa ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha utoaji wa elimu.

“Mpango huu ni fursa muhimu kwa viongozi wa shule kupata maarifa ya kisasa ya uongozi, utawala bora na usimamizi wa elimu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku,” alisema Prof. Nombo.

Prof. Nombo ameeleza kuwa mafunzo hayo hayatawahusu wakuu wa shule pekee, bali yatawajumuisha pia wakuu wasaidizi wa shule za sekondari pamoja na Maafisa Elimu Kata kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ili kuhakikisha viongozi wote wa elimu wanakuwa na uelewa unaofanana katika kusimamia ubora wa elimu.