ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

ENDELEENI KUBORESHA MIFUMO YA UONGOZI NA UTAWALA WA SHULE ILI KUENDANA NA DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2050

05 Aug, 2026
ENDELEENI KUBORESHA MIFUMO YA UONGOZI NA UTAWALA WA SHULE ILI KUENDANA NA DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2050

Akifunga rasmi Wiki ya Ushiriki wa Uongozi wa Shule iliyofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 16 Julai, 2026, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt.  Hussein Mohammed alisema jukwaa hilo limekuwa fursa muhimu ya kuwakutanisha wadau wa elimu kwa lengo la kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kuimarisha uongozi wa shule katika mazingira yanayobadilika kutokana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya elimu ya kisasa.

 

Wiki hiyo iliratibiwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) kwa kushirikiana na African Centre for School Leadership (ACSL) kupitia VVOB, ESSA, ADEA, Mastercard Foundation na FAWE, ikiwa na lengo la kuwafikia zaidi ya viongozi wa shule 16,000 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Dkt. Hussein Mohammed alisema ushirikiano huo unatoa nafasi kwa wadau mbalimbali kuchangia mawazo yatakayosaidia kuandaa viongozi wenye weledi, ubunifu na uwezo wa kuongoza mabadiliko katika sekta ya elimu ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

 

Katika hatua nyingine, aliwataka wajumbe wa Kikosi Kazi cha Uratibu wa Sekta ya Uongozi wa Shule kinachotarajiwa kuundwa hivi karibuni kuhakikisha wanatimiza majukumu yao. Kikosi hicho kitawakutanisha taasisi za serikali, vyuo vikuu, washirika wa maendeleo kwa lengo la kuratibu afua mbalimbali, kushirikishana maarifa na kuhakikisha maboresho ya uongozi wa shule yanawafikia viongozi wote nchini.

 

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid, alisema kuwa kuimarisha uongozi wa shule ni msingi muhimu wa kujenga mfumo wa elimu unaozalisha wahitimu wenye maarifa, ubunifu na uwajibikaji.

 

Alisema mazingira ya sasa yanahitaji viongozi wa shule wenye uwezo wa kuongoza kwa ufanisi, kusimamia mabadiliko,  sanjari na kutumia rasilimali zilizopo na kujenga ushirikiano madhubuti na jamii.

 

Jukwaa hili limekuwa muhimu kwa kuwakutanisha viongozi wa elimu, watafiti, wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Tanzania, kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja, na kuibua mikakati itakayochochea maboresho ya uongozi na usimamizi wa shule kwa maendeleo ya elimu nchini.