ADEM YASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI.
🗓️ 03 Juni, 2026
📍Bagamoyo, Pwani
Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) umeungana na wadau mbalimbali wa mazingira kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani katika Kampasi ya ADEM Bagamoyo ikiwa na kauli mbiu isemayo "Dira 2050 tuwajibike kukijanisha Tanzania". Maadhimisho hayo yalifanyika leo katika ukumbi mkuu wa ADEM na kuhudhuriwa na wananchi, wanachuo pamoja na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na uhifadhi wa mazingira.
Maadhimisho hayo yalitanguliwa na zoezi la upandaji miti katika eneo la ADEM, lililoongozwa na Mgeni Rasmi, Bi. Stella Msofe, Katibu Tawala wa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo. Baada ya zoezi hilo, mgeni rasmi alipata fursa ya kuzungumza na wanajamii na wanachuo wa ADEM kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Bi. Stella Msofe, alisema kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi na kwamba usafi unapaswa kuwa sehemu ya utamaduni na maisha ya kila siku ili kuhakikisha Mji wa Bagamoyo unabaki kuwa safi na salama kwa wote.
> “Tunapaswa kutambua kuwa sisi wana Bagamoyo, kila siku ndani ya mioyo yetu usafi uwe utamaduni na iwe tabia yetu. Tukubali kuwa na tabia ya usafi. Bagamoyo inapaswa kuwa safi; usafi unaanza na mimi na unaanza na wewe,” alisema Bi. Msofe.
Aidha, aliwashukuru wadau wote wa mazingira katika Mji wa Bagamoyo kwa kuungana na wananchi pamoja na jamii ya ADEM katika zoezi la upandaji miti na uwekaji wa vifaa vya kuhifadhia taka katika maeneo mbalimbali yenye msongamano wa watu. Alisisitiza kuwa kila taasisi ina wajibu wa kuhakikisha inakuwa na miundombinu stahiki ya kuhifadhi taka na kufanya usafi wa mazingira mara kwa mara.
Kwa upande wake, Naibu Mtendaji Mkuu anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi wa ADEM, Dkt. Lucas Mzelela, ambaye alikuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo ngazi ya wilaya, alitoa shukrani zake za dhati kwa mgeni rasmi na ujumbe wake kwa kushiriki na kufanikisha maadhimisho hayo.
Dkt. Mzelela aliahidi kuwa ADEM itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo katika juhudi za kuhifadhi mazingira na kuhakikisha mji huo unakuwa safi wakati wote. Vilevile, alisisitiza kuwa miti yote iliyopandwa katika kampasi ya ADEM itatunzwa kwa umakini ili kufikia malengo ya uhifadhi wa mazingira.
“Tunawashukuru sana kwa kufika na kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani katika eneo letu la ADEM. Kiukweli tumefarijika sana na tunaahidi kuwa miti hii iliyopandwa leo itatunzwa kwa umakini mkubwa,” alisema Dkt. Mzelela.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wa mazingira wakiwemo wananchi wa Mji wa Bagamoyo, wanachuo wa ADEM, wawakilishi kutoka Tanzania Forest Services Agency (TFS), National Environment Management Council (NEMC), Bagamoyo Sugar Limited pamoja na taasisi nyingine mbalimbali, wakionesha mshikamano katika juhudi za kuhifadhi na kuboresha mazingira kwa maendeleo endelevu.
