ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

ADEM YAIMARISHA MTANDAO WA WADAU WA ELIMU KUPITIA MAZUNGUMZO YA KIMKAKATI NA OPPORTUNITY EDUCATION TANZANIA.

03 Jun, 2026
ADEM YAIMARISHA MTANDAO WA WADAU WA ELIMU KUPITIA MAZUNGUMZO YA KIMKAKATI NA OPPORTUNITY EDUCATION TANZANIA.

🗓️ 02 Juni, 2026

📍Bagamoyo, Pwani

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) imeendelea kupanua wigo wa ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya elimu baada ya kufanya kikao maalum cha utambulisho na majadiliano na taasisi ya Opportunity Education Tanzania, hatua inayolenga kubaini maeneo mapya ya ushirikiano kwa ajili ya kuboresha ubora wa elimu ya sekondari nchini Tanzania.

 

Aidha kikao hicho kilichofanyika  ADEM Kampasi ya Bagamoyo na kuongozwa na Naibu Mtendaji Mkuu-Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Dkt. Lucas Mzelela ambacho kililenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu majukumu, vipaumbele na maeneo ya kazi ya taasisi hizo mbili, sambamba na kutafuta fursa za ushirikiano zitakazochangia maendeleo ya elimu nchini.

 

Katika majadiliano hayo, Opportunity Education Tanzania ilipata nafasi ya kuwasilisha dira yake, uzoefu wake wa kimataifa pamoja na utekelezaji wa programu zake nchini Tanzania kupitia mfumo wa "Quest Forward Learning", unaosisitiza ujifunzaji shirikishi, ukuzaji wa stadi na ushiriki mkubwa wa wanafunzi katika mchakato wa kujifunza.

Kwa upande wake, ADEM iliwasilisha majukumu yake ya msingi katika kuendeleza uongozi na usimamizi wa elimu, ikieleza programu mbalimbali za mafunzo, kozi fupi za maendeleo ya kitaaluma pamoja na mchango wake katika kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Elimu ya Tanzania kupitia kampasi zake za Bagamoyo, Mwanza na Mbeya.

 

Ushirikiano kati ya ADEM na Opportunity Education Tanzania unatarajiwa kufungua fursa mpya za ubunifu katika elimu, kuimarisha uwezo wa viongozi wa shule na walimu, na hatimaye kuchangia katika kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya elimu nchini Tanzania.