ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

ADEM NA CHINA KUSHIRIKIANA KUKUZA ELIMU YA KIDIJITALI

21 Sep, 2026
ADEM NA CHINA KUSHIRIKIANA KUKUZA ELIMU YA KIDIJITALI

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal University cha nchini China, wanaendesha mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo viongozi wa elimu kutoka Vyuo vya Ualimu, Wizara ya Elimu (WyEST), Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na watumishi wa ADEM kuhusu matumizi sahihi ya Akili Bandia (AI) na elimu ya Sayansi na Teknolojia (STEM) katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 1-2 Septemba, katika makao makuu ya taasisi ya ADEM mjini Bagamoyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya ADEM, Dkt. Hillary Dachi, amesema teknolojia hiyo imekuwa sehemu ya maisha ya sasa na ina uwezo wa kubadili na kuboresha namna ya kufundisha, kujifunza na kusimamia elimu.

“Akili Bandia si dhana ya siku zijazo tena, bali ni uhalisia unaobadilisha namna tunavyoishi, tunavyofanya kazi na tunavyojifunza”. Amesema Dkt. Dachi

Ameongeza kuwa, elimu ya STEM ni muhimu katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri kwa kina, kutatua matatizo na kuwa wabunifu, akisisitiza kuwa AI na STEM ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ushindani wa wanataaluma wa Tanzania katika dunia ya kidijitali.

Nae Mtendaji Mkuu ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid, amesema maendeleo ya teknolojia yameifanya sekta ya elimu kuhitaji viongozi wenye ujuzi wa kidijitali na uwezo wa kutumia teknolojia kwa uwajibikaji.

“Mafanikio ya mafunzo haya ni pale ambapo washiriki mtaenda kuyatumia maarifa mtakayoyapata katika maeneo yenu ya kazi, kwa kubaini changamoto na kutumia teknolojia kutafuta suluhisho katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji” Amesisitiza Dkt. Maulid

Dkt. Maulid amesema, mafunzo hayo ni matokeo ya ushirikiano kati ya ADEM na Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal ulioanza rasmi Desemba 29, 2023.

Aidha, amesisitiza kuwa ADEM itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi katika kujenga uwezo wa viongozi na wataalamu wa elimu.

Amesema mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kujenga mfumo wa elimu unaoendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya karne ya 21.