ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

WAZIRI MKENDA APIGIA CHAPUO MAFUNZO YANAYOTOLEWA NA ADEM

26 Nov, 2022
WAZIRI MKENDA APIGIA CHAPUO MAFUNZO YANAYOTOLEWA NA ADEM

ADEM Bagamoyo, 25 Novemba, 2022

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda ameunga mkono na kuipongeza ADEM kwa utoaji wa mafunzo ya Uongozi, Usimamizi na Uthibiti Ubora wa Elimu yanayojenga umahiri kwa walimu, na wadau wengine wa elimu katika nyanja ya Uongozi, Usimamizi na Uthibiti Ubora wa Elimu nchini.

Prof. Mkenda ameyasema hayo novemba, 25, 2022 katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Sera na Tafiti kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Ladislaus Mnyone aliyemwakilisha Mhe Waziri Mkenda katika Mahafali ya 30 ya ADEM yaliyofanyika ADEM Bagamoyo.

Akizungumza na wahitimu katika mahafali hayo kwa niaba ya Waziri Mkenda, Prof. Mnyone amesema ADEM imejizatiti na inafanya kazi nzuri katika kuboresha mazingira ya utoaji mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu pamoja na Uthibiti Ubora wa Shule hivyo Walimu waliohitimu mafunzo hayo wamepikwa na kuiva katika eneo la Uongozi, Usimamizi na Uthibiti Ubora wa Elimu.

“Ninaipongeza ADEM kwa kuendesha kozi mbalimbali zikiwemo za Astashahada na Stashahada na ubunifu wa uandaaji wa Mtaala wa Shahada ya Usimamizi wa Uthibiti Ubora wa Elimu ili kuendana na mabadiliko ya kisekta na kuimarisha utendaji kazi katika ngazi mbalimbali za elimu” Amesema Prof Mnyone

Ameongeza, ninaielekeza Menejimenti ya ADEM, kuendelea kuboresha mafunzo ya Muda Mfupi na Muda Mrefu, kwa kuzingatia mahitaji ya soko na mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika sekta ya elimu huku akitanabaisha kuwa Wizara itaendelea kufanya uboreshaji wa miundombinu ya ujifunzaji na kufundishia kwa kutoa rasilimali fedha na ushauri ili kuhakikisha inakijengea Chuo uwezo zaidi wa kutoa mafunzo.

Nae Mtendaji Mkuu w ADEM, Dkt. Siston Masanja Mgullah akizungumza katika Mahafali hayo amesema jumla ya Walimu 869 wamehitimu mafunzo yao ambapo Wahitimu 699 ni wa Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu (DEMA), wahitimu 169 ni wa Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule na Mhitimu mmoja amehitimu mafunzo ya Astashahada ya Uongozi, Usimamizi na Utawala wa Elimu (CELMA)

“Ni mategemeo yetu ni kuwa, wahitimu wa kozi ya Uongozi na Usimamizi wa elimu kwa ngazi za Astashahada na Stashahada wataongoza vizuri shule, kupanga mipango inayotekelezeka, kusimamia utekelezaji wa mtaala pamoja na upimaji wa maendeleo ya wanafunzi kwa umahiri” Amesema Dkt Masanja.

Ameongeza kuwa, wahitimu wa kozi ya Uthibiti Ubora wa Shule wana uwezo wa kuunda timu za uthibiti ubora wa shule, kuandaa vigezo vya shule fanisi na kufanya ufuatiliaji wa karibu wa shughuli za shule ikiwemo ufundishaji na ujifunzaji na kuzisaidia shule kuimarisha tahadhari dhidi ya majanga kama vile moto ili kupunguza athari za zake shuleni.

Bw. Emmanuel Qeresh mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya ADEM katika Mahafali ya 30 ya ADEM akizungumza kwa niaba ya Wahitimu wenzake amesema, Mafunzo waliyoyapata ADEM yatawasaidia sana kuwa Viongozi, wasimamizi na wathibiti Ubora wa Elimu mahiri katika Shule wanazosimamia.

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) unafanya shughuli zake chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ukiendesha mafunzo ya Muda Mrefu na Muda Mfupi ya Uongozi, Usimamizi na Uthibiti Ubora wa Elimu, lengo likiwa ni kuboresha Uongozi na Usimamizi wa elimu nchini katika shule za Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ualimu na kwa Maafisa Elimu wote kuanzia ngazi ya Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa.