ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

WAWEZESHAJI 256 WA MAFUNZO YA UONGOZI, USIMAMIZI NA UENDESHAJI WA ELIMU KWA WALIMU WAKUU NCHINI WAPATIWA MAFUNZO

23 Sep, 2023
WAWEZESHAJI 256 WA MAFUNZO YA UONGOZI, USIMAMIZI NA UENDESHAJI WA ELIMU KWA WALIMU WAKUU NCHINI WAPATIWA MAFUNZO

Timu ya wawezeshaji wa mafunzo ya Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu, pamoja na Utawala Bora wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wapatao 256 wamepatiwa mafunzo ya kwa siku tatu kuwaandaa kufanya uwezeshaji na kuwajengea uwezo Walimu Wakuu nchini juu ya masuala ya Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu, pamoja na Utawala Bora wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa yatakayofanyika katika Mikoa 7 ya Tanzania Bara kuanzia Septemba 26 hadi Oktoba 14, 2023.

Akizungumza katika ufungaji wa mafunzo hayo Naibu Katibu Mkuu Elimu, Dkt. Franklin Rwezimula aliyekuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya ufungaji wa mafunzo hayo leo Septemba 23, 2023 ADEM Bagamoyo, ameipongeza Menejimenti ya ADEM chini ya uongozi wa Dkt. Siston Masanja Mgullah kwa kusimamia uendeshaji wa mafunzo kwa Timu hiyo ya Wawezeshaji.

“Ni imani yangu kwamba mafunzo haya yameratibiwa na kusimamiwa vizuri, sisi kama Wizara tunathamini kazi inayofanywa na ADEM katika kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu nchini, ninawasihi muendelee kufanya kazi hii kwa umahiri huo huo ili mtimize malengo ya kuanzishwa kwa Wakala huu. Mafunzo haya yaendelee kuzifanya taasisi zetu za elimu hususani Shule, kuwa na viongozi mahiri wanaoweza kuongoza na kusimamia ufundishaji na ujifunzaji nchini”. Amesema Dkt. Rwezimula.

Ameongeza kuwa, Wizara inatambua kuwa pamoja na vigezo vingine, suala la Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu lina mchango mkubwa katika maendeleo ya Shule na elimu kwa ujumla, Uongozi bora wa Shule unasaidia kuimarisha usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji, kusimamia vizuri rasilimali za Shule, kusimamia miradi vizuri, kuboresha Uthibiti Ubora wa Shule na kufanya maamuzi sahihi na yenye tija. Serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa katika Sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha Mitaala, kuhuisha Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, kuajiri Watumishi wapya, kujenga na kukarabati miundo mbinu ya Shule.

Dkt. Rwezimula amesisitiza kusimamiwa vizuri kwa Mabadiliko na maboresho hayo ili kufanikisha adhma ya Serikali vizuri katika kuboresha elimu nchini na kuongeza kuwa katika mabadiliko hayo ADEM ina wajibu mkubwa wa kuisaidia Serikali kufikia malengo ya mabadiliko ya elimu kwa kutoa mafunzo na kufanya Tafiti ili kuboresha Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu nchini.

Naye Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Siston Masanja Mgullah amesema, mafunzo hayo yamelenga kuiandaa Timu hiyo ya Wawezeshaji 256 kwenda kufanya uwezeshaji kwa Walimu Wakuu 4,516 katika Mikoa ya Dar Es Salaam, Pwani, Morogoro, Njombe, Songwe, Dodoma na Mara.

“Tumedhamiria kuhakikisha kuwa mafunzo haya yanakuwa na tija na uendelevu kwani Timu hii imehusisha Maafisa Elimu Taaluma kutoka katika Mikoa yote 7 itakayohusika katika mafunzo na Maafisa elimu Taaluma, Vifaa na Takwimu, Elimu ya Watu Wazima ngazi ya Halmashauri zitakazohusika katika mafunzo haya" Amesema Dkt. Masanja.

Dkt. Masanja amewataka Wawezeshaji hao kwenda kuwajengea uwezo Walimu Wakuu nchini katika ya masuala ya Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu, pamoja na Utawala Bora wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa umahiri mkubwa ili kuisadia Serikali kufikia malengo ya kuwawezesha Walimu Wakuu kuwa na uwezo wa kupanga mipango ya kimkakati ya kuimarisha uendeshaji wa elimu hususani katika maeneo ya Usimamizi wa Ufundishaji na ujifunzaji, Utawala Bora, Usimamizi wa Rasilimali, Miiko na maadili ya kazi, kushughulikia malalamiko ya walimu vizuri na kwa haki na kusimamia usalama wa Watoto.  

Aidha, Dkt. Masanja amesisitiza Timu hiyo ya Wawezeshaji kujiamini na kujenga mtazamo chanya katika kutekeleza wajibu wao kwani kazi hiyo itakuja kupimwa ufanisi wake kwa Walimu Wakuu watakaopatiwa mafunzo hayo katika namna watakavyokuwa wakitekeleza majukumu yao mara baada ya kujenegewa uwezo juu ya kama kigezo katika mradi wa BOOST.

 

Bw. Alfred J. Shangwe aliyeshiriki mafunzo hayo akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake amesema wapo tayari kwenda kufanya uwezeshaji kwa ufanisi, kwani mbinu zilizotumika katika kuwajengea uwezo ni mbinu rafiki na wao wamezichukua ili ziwasaidie kwenda kuwawezesha Walimu Wakuu katika vituo watakavyopangiwa kwa umahiri ule ule waliopokea kutoka kwa Timu ya Kitaifa ya Waweweshaji na hatimaye kufikia lengo la Serikali la kuwajengea uwezo Walimu Wakuui ili waweze kutekeleza majukumu yao ya Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Elimu nchini kwa ufanisi mkubwa.  

Mafunzo haya yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 21-23, 2023 ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa BOOST, kupitia Afua namba 8 ambayo inalenga kuimarisha Utawala Bora wa Elimu katika ngazi ya Shule na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kupitia mafunzo hayo Walimu Wakuu watajengewa umahiri wa kusimamia shughuli za uendeshaji wa Shule na Afua zingine za mradi lakini pia ADEM imeandika vitabu viwili, cha Kiongozi cha Mwalimu Mkuu na Utawala Bora wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ambavyo vyote vimeandaliwa chini ya ufadhili wa mradi wa BOOST chini ya Benki ya Dunia.