ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

WALIMU WAKUU 608 WA MKOA WA PWANI KUPATIWA MAFUNZO KUIMARISHA UONGOZI, USIMAMIZI NA UENDESHAJI WA SHULE

29 Sep, 2023
WALIMU WAKUU 608 WA MKOA WA PWANI KUPATIWA MAFUNZO KUIMARISHA UONGOZI, USIMAMIZI NA UENDESHAJI WA SHULE

Walimu Wakuu 365 kutoka katika Halmashauri za Chalinze, Bagamoyo, Kibaha mji, Kibaha vijijini, Kibiti na Rufiji wameshiriki mafunzo maalumu ya Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Shule pamoja na Utawala Bora wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa yanayoendeshwa na ADEM katika Mikoa 7 nchini ambapo awamu ya kwanza ya mafunzo hayo imehusisha walimu wakuu kutoka Mkoa wa Pwani, Dar Es Salaam, Njombe, Dodoma, Morogoro, Mara na Songwe.

Awamu ya kwanza ya mfunzo hayo kwa Mkoa wa Pwani imekamilika yakianzia katika Mkoa wa Pwani Mafunzo yanayoendelea kutolewa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu Septemba 28, 2023 baada ya Walimu Wakuu hao 608 kujengewa uwezo kwa muda wa siku tatu juu ya masuala ya Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Shule pamoja na Utawala Bora wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. 

Akifunga awamu hiyo ya kwanza ya mafunzo kwa Walimu Wakuu wa Mkoa wa Pwani, Naibu Katibu Mkuu Elimu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula amesema Uongozi bora wa Shule unasaidia kuimarisha usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji, kusimamia rasilimali za Shule, utekelezaji wa miradi, kuboresha Uthibiti Ubora wa Shule na kufanya maamuzi sahihi yenye tija.

Dkt. Rwezimula ameongeza kuwa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inathimini mchango wa ADEM katika kuimarisha Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Shule  na elimu kwa ujumla hapa nchini.

“ADEM ina wajibu wa kuisaidia Serikali kufikia malengo ya mabadiliko ya elimu kwa kutoa mafunzo na kufanya utafiti ili kuimarisha Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Shule na Elimu kwa ujumla”

Aidha,  Dkt. Rwezimula amewataka washiriki wa mafunzo hayo kubadilika kutokana na namna walivyopata mafunzo na kujengewa uwezo katika maeneo mbalimbali.

“Tunatarajia kuona mabadiliko chanya na endelevu katika uendeshaji wa shule. Matokeo ya mafunzo yatapimwa katika utendaji wenu kupitia viashiria vya ufanisi ,kama hakutakuwa na mabadiliko basi utakuwa ni upotevu wa rasilimali fedha na muda” amesisitiza Dkt. Rwezimula

Kwa upande wake Naibu Mtendaji Mkuu Taaluma ADEM, Dkt. Alphonce Amuli amesema, mafunzo yaliyotolewa yamelenga kuimarisha utendaji kazi wa Walimu Wakuu hao na kuwapa uwezo wa kuyamudu majukumu mapya na majukumu waliyonayo awali ambayo walikuwa wanayatekeleza kwa uzoefu na si ufanisi.

Dkt. Amuli ameeleza kuwa, mara baada ya mafunzo hayo kukamilika hatua ya ufuatiliaji na tathimini itafanyika katika shule ambazo wanatoka washiriki hao kupima ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Walimu Wakuu kwa kuzingatia walichojifunza na viashiria vya ufanisi na umahiri.

“Tunatarajia kuona mabadiliko baada ya mafunzo kwa yale yote ambayo wamefundishwa huku zoezi la ufuatiliaji likifanyika katika shule ambazo washiriki wa mafunzo wametoka kuona kama kuna mabadiliko yametokea” amesema Dkt. Amuli.

Akitoa taarifa fupi ya mafunzo hayo, mratibu wa mafunzo Bw. Richard Sungura amesema mafunzo hayo yanaendeshwa kwa awamu mbili kwa walimu wakuu 608 katika Halmashauri zote 9 za Mkoa wa Pwani ambapo awamu ya kwanza ya mafunzo imeanza Septemba 26, 2023 hadi Septemba 28, 2023 kwa washiriki kutoka Halmashauri za Chalinze, Bagamoyo, Kibaha mji, Kibaha vijijini, Kibiti na Rufiji.

Sungura ameongeza kuwa, awamu ya pili ya mafunzo itaanza siku ya Ijumaa Septemba 29, 2023 hadi tarehe 01 Oktoba, 2023 na kushirikisha Walimu Wakuu 243 kutoka Halmashauri za Kisarawe, Mkuranga na Mafia.

Akiongea kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo Bw. Maulidi Ramadhan ameshukuru kwa nafasi hiyo ya kupata mafunzo na kuahidi kuwa yatakwenda kuongeza tija katika kusimamia shughuli mbalimbali za uendeshaji wa shule, ufundishaji na ujifunzaji pamoja na uongozi bora wa elimu Shuleni.

Mafunzo ya uongozi na usimamizi wa shule pamoja na utawala bora katika elimu kwa walimu wakuu kutoka Mkoa wa Pwani yanalenga kuwajengea uwezo walimu wakuu katika kutekeleza majukumu yao ya kusimamia uendeshaji wa Shule kwa ubora na ufanisi.

Walimu Wakuu hao wanajengewa umahiri katika maeneo ya Uongozi, Usimamizi na Uendeshaji wa Shule, Utawala Bora katika elimu, Uendeshaji wa ofisi ya Mwalimu Mkuu, Utunzaji wa kumbukumbu shuleni, Ukusanyaji wa takwimu na uandaaji wa mpango wa ujumla wa maendeleo ya shule, Motisha kwa wafanyakazi, Usimamizi wa Ufundishaji na Ujifunzaji kwa ufanisi shuleni, Usimamizi wa rasilimali vitu shuleni, Ustawi na usalama wa wanafunzi shuleni, Ufuatiliaji na usimamizi wa ufanisi wa shule, Usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya shule na Ushirikishwaji wa jamii katika utatuzi wa malalamiko katika elimu