ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

WALIMU WAKUU 170 WA SHULE ZA MSINGI ZA JIJI LA DAR ES SALAAM KUPATIWA MAFUNZO YA UONGOZI NA USIMAMIZI WA SHULE

10 May, 2023
WALIMU WAKUU 170 WA SHULE ZA MSINGI ZA JIJI LA DAR ES SALAAM KUPATIWA MAFUNZO YA UONGOZI NA USIMAMIZI WA SHULE

Walimu Wakuu wa Shule za Msingi za Serikali na binafsi za Jiji la Dar Es Salaam ambao pia ni wanachama wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania - TAPSHA leo Mei wameanza mafunzo ya siku tatu ya Uongozi na Usimamizi wa Shule yenye lengo la kuwajengea uwezo wa Uongozi na Usimamizi wa Shule wanazozisimamia Walimu Wakuu hao.

Mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoratibiwa na Ofisi ya Mkurugenzi Jiji la Dar Es Salaam yanafanyika ADEM Bagamoyo kuanzia Mei 10 -12, 2023 ambapo wataalam wa ADEM watafanya uwezeshaji kwa walimu hao wapatao 170.

Akifungua mafunzo hayo mlezi wa TAPSHA Jiji ambaye pia ni Afisa Elimumsingi Jiji la Dar Es Salaam, Bi. Spora Tenga ameupongeza Uongozi wa ADEM kwa utayari wa kuendesha mafunzo hayo na kuwaasa washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanazingatia mada zote zitakazofundishwa.

Aidha, Mtendaji Mkuu Dkt. Siston Masanja Mgullah akizungumza wakati wa ufunguzi amesema elimu bora inaletwa na viongozi bora wa elimu, hivyo mafunzo hayo yawasaidie walimu wakuu hao kutekeleza majukumu yao ya Uongozi na Usimamizi wa shule.

“Nendeni mkafanyie kazi maarifa na ujuzi mtakaopata, mafunzo haya yawe chachu ya kubadilisha mtazamo wa utendaji kazi wenu, yawasaidie kuwa na mtazamo chanya katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku na yatakapokamilika kila mshiriki ajipime kama amepata maarifa, ujuzi wa kutosha na namna yatakavyomsaidia kuleta mabadiliko chanya katika Uongozi na Usimamizi wa Shule anayoisimamia”. Amesema Dkt. Masanja.

Nae Mwenyekiti wa TAPSHA Jiji la Dar Es Salaam, Bw. Godrick Rutayungururwa akizungumza na Walimu Wakuu hao amesema mafunzo hayo yanafanyika chini ya ufadhili wa Ofisi ya Mkurugenzi Jiji la Dar Es Salaam, hivyo amewasihi washiriki kuwa wasikivu ili tija ya mafunzo hayo na thamani ya fedha itakayotumika kuendesha mafunzo hayo ionekane.

Awali ya yote, Katibu wa TAPSHA Jiji la Dar Es Salaam Bw. Simon Mdendemi amesema ni matarajio yao kuwa baada ya mafunzo walimu wakuu wataweza kuongoza na kusimamia vema shule na kuzuia migogoro mahali pa kazi, kuandika maandiko mradi, kuandaa harambee pamoja na kuwa na uelewa wa itifaki na kutoa huduma bora kwa wateja.

Mwalimu Vallence Evarist Hagila na Mwalimu Hadija Abbas Kimbunga ambao ni washiriki wa mafunzo hayo wakizungumza baada ya ufunguzi huo wamesema, wanaamini kuwa ADEM ina wataalam mahiri watakaofanya uwezeshaji stahiki wa mada zilizoandaliwa na mafunzo haya yatapelekea mabadiliko makubwa katika utendaji kazi wao.