VYUO VYA MAENDELEO YA WANANCHI FDC, ZINGATIENI UTOAJI WA ELIMU UJUZI KWA VIWANGO BORA: MKURUGENZI WA ELIMU YA UFUNDI -WyEST

Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Fredrick Salukele ameutaka Uongozi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu kuhakikisha wanaimarisha mifumo ya utoaji elimu ujuzi katika viwango bora kwa wananchi wanaowahudumia ili jamii ivutiwe kujiendeleza kiujuzi kwenye mafunzo yanayotolewa kwenye vyuo hivyo.
Ameyasema hayo leo Julai 03, 2025 wakati alipokuwa akifungua mafunzo maalumu ya uongozi, usimamizi na utawala Bora wa Elimu yanayolewa na ADEM kwa Menejimenti ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu yanayofanyika ADEM Bagamoyo kwa siku mbili yakilenga kuwajengea uwezo viongozi hao kuhusu kutoa huduma bora kwa wananchi wanahitaji kupata huduma kupitia Chuo hicho.
“Utoaji wa huduma bora unahusisha usimamizi thabiti wa elimu inayotolewa, kuimarisha Utawala bora wa elimu katika Vyuo vyetu, kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa wananchi wanaojiendeleza katika vyuo vyetu na kuhakikisha kunakua na uthibiti ubora wa elimu inayolewa” Amesema Dkt. Salukele
Dkt. Salukele ameongeza kuwa ni muhimu kwa Chuo kuimarisha uthibiti ubora katika mafunzo yanayotolewa na Chuo hicho yakihusisha elimu ujuzi kwani mwelekeo wa Serikali kwa sasa kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 linasisitiza elimu ujuzi na kujitegemea na Vyuo vyote vya Maendeleo ya Wananchi vinahusika moja kwa moja na kuzalisha wahitimu wenye ujuzi utakaowawezesha kujiajiri katika sekta mbalimbali.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu-ADEM Dkt. Maulid J. Maulid ameupongeza uongozi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu kuona umuhimu wa kupata maarifa kuhusu uongozi na usimamizi wa elimu kupitia ADEM katika kipindi hiki cha maboresho makubwa katika sekta ya elimu yanayolenga kuimarisha elimu ujuzi kwani mafunzo hayo yatawasaidia kwenda kufanya usimamizi mahiri wa elimu inayotolewa na Chuo hicho.
Dkt. Maulid ameongeza kuwa ADEM imejipanga kuwanoa viongozi hao katika eneo la uongozi, usimamizi na Utawala Bora wa Elimu ili wakatekeleze majukumu yao kwa ufanisi na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ione tija ya Wakala kuendelea kuwa kinara katika utoaji wa mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa elimu kwa viongozi wa Elimu nchini.
“Tunaishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuendelea kuuwezesha Wakala katika utoaji wa mafunzo ya uongozi, usimamizi na utawala Bora wa elimu kwa viongozi mbalimbali wa elimu nchini, kwa upande wa mafunzo haya tutakayowapatia viongozi haw awa elimu kutoka Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu, Wakala utahakikisha unawajengea uwezo kuhusu masuala muhimu ya kuzingatia katika kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu katika Chuo chao ili tija ya kutolewa kwa mafunzo hayo ionekane”. Amesisitiza Dkt. Maulid.
Nae Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu Bi.Fridegarda Mukyanuzi ambaye ameambatana na viongozi wengine wa Chuo hicho kushiriki katika mafunzo hayo yanayotolewa na ADEM amesema kuwa ADEM ni mahali sahihi kwa kuchota maarifa kuhusu uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shughuli za elimu, hivyo wana amini baada ya kupatiwa mafunzo hayo watarudi wakiwa na maarifa mapya yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi hususani kuimarisha utoaji wa elimu ya ujuzi na kujitegemea katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kasulu.