VIONGOZI WA ELIMU 1014 WAPATIWA MAFUNZO YA UONGOZI WA ELIMU MKOANI MTWARA.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewataka Maafisa Elimu Kata na Walimu Wakuu waliohitimu mafunzo ya Uongozi na Usimamizi fanisi wa Shule kuitumia elimu waliyopata kuongeza ufanisi katika sekta ya elimu mkoani humo.
Kanali Abbas ameyasema hayo katika hafla ya kuwatunukia vyeti wahitimu 1014 wa mafunzo hayo iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Mustapha Sabodo, Februari 13, 2023 ambapo amebainisha kuwa anaamini ujuzi walioupata utachangia kuboresha utendaji kazi wao ikiwa ni pamoja kuwaongezea mbinu na umahiri wa kitaaluma ili kuusaidia Mkoa kufikia malengo yake ya kupandisha kiwango cha ufaulu.
“Nina furaha kubwa kukabidhi vyeti hivi kwa Maafisa Elimu na Walimu Wakuu walioshiriki mafunzo haya kutoka katika Halmashauri zetu tisa za Mkoa wa Mtwara. Nina imani kuwa mafunzo haya yana tija na yataongeza ufanisi katika utendaji kazi wenu na hivyo yatasaidia kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika Mkoa wetu. Kanali Abbas pia amewataka wahitimu wote wa mafunzo hayo kutekeleza kwa vitendo elimu waliyopatiwa na kuitumia kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya Elimu Mkoani Mtwara. “Amesema Kanali Abbas”.
Aidha Kanali Abbas ameipongeza ADEM, kwa kukubali kutoa mafunzo hayo na kusema kuwa Serikali ya Mkoa itahakikisha inawasimamia na kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa viongozi wote waliopatiwa mafunzo hayo ili waweze kwenda sambamba na malengo ya mafunzo hayo na kuongeza kuwa Mkoa wa Mtwara utajipanga kuhakikisha kuwa mafunzo hayo yanaendeshwa kila mwaka.
ADEM iliendesha hayo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule Mkoani Mtwara kwa muda wa wiki tatu yakiwashirikisha Wakuu wa Shule za Awali na Msingi, Sekondari na Maafisa Elimu Kata wapatao 1014 baada ya Uongozi wa Mkoa wa Mtwara kufanya ubainishaji wa changamoto zinazoikabili sekta ya elimu Mkoani humo baada ya Mkoa huo kuwa na historia ya kutofanya vizuri kitaaluma na moja ya jitihada zilizofanyika kuondokana na changamoto hiyo ni kuendesha mafunzo hayo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule yaliyolenga kuimarisha na kusimamia ufundishaji na ujifunzaji ambapo yaliendeshwa katika kanda tatu ambazo ni Masasi, Newala na Mtwara kuanzia tarehe 5 -22 Disemba, 2022 na kujumuisha jumla ya washiriki 1014 kati ya 1025 sawa na 99% ya walengwa wa mafunzo hayo. Viongozi waliopatiwa mafunzo hayo ni Wakuu wa Shule za Awali na Msingi 678, Wakuu wa Shule za Sekondari 152 na Maafisa Elimu Kata 184