ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

VIONGOZI 13 WA IDARA YA ELIMU SMZ WAHITIMISHA MAFUNZO YA UONGOZI ADEM

29 Aug, 2022
VIONGOZI 13 WA IDARA YA ELIMU SMZ WAHITIMISHA MAFUNZO YA UONGOZI ADEM

Viongozi kumi na tatu (13) kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wamekamilisha mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Skuli pamoja na Uandaaji wa mpango mkakati wa elimu yaliyotolewa na Wakala kwa Viongozi hao wanaotokea Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo Mtendaji Mkuu Dkt. Siston Masanja Mgullah ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuona umuhimu wa kuwaleta Viongozi hao ADEM kuja kupatiwa mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Skuli.

“Tunamshukuru sana Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuona umuhimu wa mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu yanayotolewa na ADEM kwa Viongozi mbalimbali wa Elimu nchini na Umuhimu wa mafunzo haya umepelekea kuridhia mafunzo haya kuendeshwa kwa viongozi kumi na tatu (13) wa Elimu kutoka Wizara anayoisimamia ili kuhakikisha Usimamizi bora wa Skuli zinazosimamiwa na Wizara yake” Amesema Dkt. Masanja

Aidha Dkt. Masanja ametoa rai kwa viongozi hao kumi na tatu (13) waliopatiwa mafunzo hayo kuhakikisha wanakwenda kutekeleza kwa weledi majukumu yao ya usimamizi wa Skuli kwani kupitia mafunzo waliyopata ADEM sasa wana ujuzi na maarifa ya kutosha kuleta mabadiliko chanya ya ufundishaji na ujifunzaji.

“Nendeni mkawe chachu ya mabadiliko na chanzo cha kuleta mafanikio katika Sekta ya elimu kule mnakofanya kazi, mkaongeze usimamizi wa Skuli, mfanye tathmini iwapo Skuli mnazosimamia zina mipango mikakati inayoendana na mazingira halisi ya Skuli, kasimamieni kwa ukaribu nidhamu ya walimu na wanafunzi, wapeni walimu motisha kwani haya yote yanalenga kuleta matokeo chanya katika ustawi wa elimu hasa ufaulu wa wanafunzi” Amesema Dkt. Masanja.

Nae naibu Mtendaji Mkuu Taaluma, Dkt. Alphonce J. Amuli amewataka Viongozi waliopatiwa mafunzo hayo kuyatilia mkazo na kwenda kuyatekeleza kwa vitendo hasa kwa kuzingatia mazingira waliyopo ili yalete tija iliyokusudiwa na kuwaomba wasichoke kujifunza mara kwa mara kwani kiongozi bora ni yule asiyechoka kujifunza mambo mapya kila wakati.

Kadhalika Meneja wa Programu za mafunzo Bi. Basiliana Mrimi amesema baadhi ya maeneo ambayo viongozi hao wamejengewa umahiri ni maeneo ya uongozi na usimamizi wa elimu, namna ya kuandaa mpango mkakati, haiba za kazi, kusimamia itifaki, na namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo kazini.

Aidha, Mratibu wa mafunzo ya muda mfupi, Bw. Ombeni Mbwilo pia amewaeleza Viongozi hao kuwa, ADEM ina wataalam wa kutosha waliojaa maarifa katika nyanja za Uongozi na Usimamizi wa elimu hivyo kuwaomba kuwahimiza fursa walimu wanaowasimamia kujiunga na ADEM kwa mafunzo ya muda mrefu ya Stashahada za Uongozi na Usimamizi wa Shule na Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule kwani mafunzo hayo yatawaandaa walimu hao kuwa Viongozi katika sekta ya elimu na Uthibiti Ubora wa Skuli zao  pale watakapohitimu mafunzo hayo na watakuwa na mchango mkubwa katika kuinua ubora wa elimu katika Skuli zao.

Bw. Mbwilo pia ametumia fursa hiyo kuwaalika Walimu na viongozi wa elimu kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mafunzo ya muda mfupi ya Uongozi na Usimamizi wa elimu yatakayoendeshwa kwa mwezi mmoja ifikapo Mwezi Disemba 2022, na kufafanua kuwa ada ya kushiriki mafunzo hayo itakuwa Shilingi Mia saba na arobaini elfu tu (750,000/-) kwa mtu mmoja.

Nae Bw. Mfaume Jafari Mfaume akizungumza kwa niaba ya wanamafunzo wenzake walioshiriki mafunzo hayo ameipongeza ADEM kwa uwezeshaji bora uliokidhi mahitaji yao kwa Asilimia mia moja na kukiri kuwa kwa siku tano walizokaa ADEM wameshiba maarifa na ujuzi katika Uongozi na Usimamizi wa Skuli na wapo tayari kwenda kusababisha mabadiliko katika maeneo wanayosimamia.

Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu kwa viongozi hao yamefanyika kwa siku tano kuanzia Agosti 25 na yamehitimika leo 29 Agosti, 2022.