Ujifunzaji na ufundishaji kwa mbinu ya michezo waongeza ufaulu, mahudhurio ya wanafunzi shuleni

Dar es Salaam
24 Septemba, 2025
Mradi wa Play matters uliotekelezwa Mkoani Kigoma umefikia tamati kwa Mafanikio ambapo ulianza kutekelezwa mnamo mwaka 2021 chini ya Shirika lisilo la Kiserikali la IRC (International Rescue Committee) na Plan International chini ya Ufadhili wa LEGO Foundation kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali ikiwemo Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) na Taasisi ya Elimu (TIE)
Mradi huu umetekelezwa kwa lengo la kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa Watoto wenye umri kati ya miaka 2 hadi 12+ kupitia mbinu ya michezo ukilenga kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira ya Makambi ya wakimbizi Mkoani Kigoma, katika wilaya za Kasulu na Kibondo pamoja na kambi za wakimbizi za Nduta na Mtendeli.
Akizungumza katika hafla ya ufungaji Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Aneth Komba aliyemwakilisha Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mutahaba aliyekuwa mgeni rasmi amesema kuwa ujifunzaji na ufundishaji kwa mbinu ya michezo nchini umesaidia kuongeza ufaulu, mahudhurio shuleni na kupunguza utoro na uchelewaji wa wanafunzi.
“Shule ya Msingi Nyarugusu, Nyachenda na Mkambati zilizopo Kasulu pamoja na shule za Katelela, Kayemba na Muyaga zilizopo Halmashauri ya Kibondo ni mfano wa shule ambazo viwango vyao vya ufaulu vimepanda, mahudhurio shuleni yameongezeka, wanafunzi wamekuwa na ari ya kupenda shule na kufika kwa wakati ili kujifunza zaidi,” amesema Komba na kuongeza
Nae Mtendaji Mkuu ADEM Dkt. Maulid J. Maulid akizungumza katika hafla hiyo amesema katika kutekeleza mradi huo, makubaliano pia yaliingiwa kati ya IRC, Plan International na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, ambazo Wakala wa Maendeleo ya Elimu (ADEM) na Taasisi ya Elimu Tanznaia (TIE) ambapo ADEM imeshiriki kuandaa matini mbili za mafunzo kuhusu majukumu ya Kamati ya Shule na matini kuhusiana na Mafunzo Endelevu kwa Walimu Kazini.
“Matini hizi zilizoandaliwa na ADEM zitamwezesha Mwalimu kupata mbinu za kuwasaidia wanafunzi kujifunza kwa njia ya michezo huku moduli ya pili itawawezesha viongozi wa shule kupata za kusimamia ufundishaji na ujifunzaji mahiri shuleni” Amesema Dkt. Maulid.
Mkuu wa Mradi huo, Bi. Juliana Nyigura amesema ‘Play Matters’ ni mpango uliotekelezwa kwa miaka mitano (2021-2025) ukilenga kufanya mabadiliko ya uzoefu wa ujifunzaji kupitia mbinu ya michezo kwa watoto zaidi ya 100,000 katika kambi za wakimbizi na jamii zinazowahifadhi wakimbizi.
“Tunayo furaha kutamka leo kuwa mradi umefanikiwa kuvuka lengo hilo. Kwa Tanzania tumewafikia watoto 103,668 kati ya 100,000 waliolengwa katika wilaya ya Kibondo na Kasulu. Takwimu hizi zinaonesha kuwa mradi umevuka malengo kwa ongezeko la watoto 3,668 ambao wamenufaika na mazingira ujifunzaji shirikishi, yanayofurahisha na salama.
“Kwa upande wa walimu, mradi umetoa mafunzo ya ujifunzaji kwa mbinu ya michezo kwa walimu 1,860. Mafunzo hayo yalilenga kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji darasani na kuimarisha uhusiano wa walimu na wanafunzi. Pia mradi uliwafikia viongozi wa kijamii 1,156 katika wilaya zote mbili kupitia hafua mbalimbali za kuwezesha ujifunzaji kwa mbinu ya michezo,” amesema Bi. Juliana.