ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

TUKO PAMOJA PROJECT YAKUSANYA MILIONI 15 ZITAKAZOTUMIKA KUJENGA VIMBWETA KAMPASI YA BAGAMOYO

18 Jul, 2022
TUKO PAMOJA PROJECT YAKUSANYA MILIONI 15 ZITAKAZOTUMIKA KUJENGA VIMBWETA KAMPASI YA BAGAMOYO

Programu iliyoandaliwa na Wanachuo wa ADEM Kampasi ya Bagamoyo iliyopewa jina la TUKO PAMOJA PROJECT imefikia kilele siku ya ijumaa Julai 15, 2022 ambapo Wanachuo hao wamefanikiwa kuendesha harambee ya kuchangisha fedha ili kufanikisha lengo la programu hiyo ambalo ni ujenzi wa vimbweta katika Kampasi ya Bagamoyo.

Akizungumza kwa niaba ya Wanachuo, mratibu wa program hiyo, Bw. George Lameck Ubuyu amesema, TUKO PAMOJA PROJECT ni programu iliyoandaliwa na Serikali ya Wanachuo wa ADEM (ASO) Kampasi ya Bagamoyo yenye lengo la kufanikisha ujenzi wa Vimbweta ili kuboresha mazingira ya kujifunzia Chuoni.

“Tunajifunza moduli ya Utafutaji wa Rasilimali kwa maendeleo ya Shule ‘Resource mobilization’ tukiwa darasani, na tumeamua kuweka kwenye vitendo yale tunayojifunza kwa kuanzisha program hii ya Ujenzi wa Vimbweta ambayo inahitaji fedha ili kuifanikisha, hivyo tumeandaa harambee hii” Amesema Bw. Ubuyu

Ameongeza, Programu ya TUKO PAMOJA PROJECT ina lengo la kuhakikisha tunajenga vimbweta 20 vitakavyokuwa vimeunganishwa na mfumo wa umeme ili kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa Wanachuo ambapo Wanachuo kwa kushirikiana na wadau wengine walio tayari kuunga Mkono programu hiyo watachangia ujenzi wa vimbweta hivyo.

Aidha, Mtendaji Mkuu ADEM, Dkt. Siston Masanja Mgullah ambaye aliongozana na Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Mjini, Mhe. Mharami Mkenge ambaye alikua mgeni rasmi katika harambee hiyo amesema, ni jambo la kujivunia sana Wanachuo hao kuyaweka mafunzo waliyoyapata darasani katika vitendo kwa kuendesha harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa vimbweta ambavyo vitatumiwa na wanachuo hao na wengine watakaokuja kusoma ADEM

“Nawapongeza sana kwa ubunifu, uwezo wa kutafsiri mlichojifunza darasani na ambavyo elimu mliyoipata ADEM imewabadili mtazamo wa namna ya kutekeleza majukumu yenu katika Shule mnazosimamia. Sisi ADEM ni mafanikio makubwa sana na tunajivunia utoaji elimu bora yenye msingi wa kuwajengea walimu uwezo katika masuala ya Uongozi ‘competence based curricullum’ na utekelezaji wa program ya TUKO PAMOJA PROJECT ni matunda ya elimu mliyoipata ADEM ni Imani yangu kuwa sasa mmeiva mpo tayari kwenda kuleta mabadiliko makubwa ya Uongozi na Usimamizi wa Shule mnazozisimamia na Sekta ya Elimu kwa ujumla” Amesema Dkt. Masanja.

Programu ya TUKO PAMOJA PROJECT ilianza kwa Wanachuo kushiriki ligi maalum ya madarasa iliyohusisha mpira wa miguu, mpira wa wavu na mpira wa pete, ikifuatiwa na mechi za mpira wa miguu, mpira wa wavu na kuvuta Kamba baina ya Wanachuo na Watumishi wa ADEM, na kilele cha programu ya TUKO PAMOJA PROJECT imehusisha Harambee iliyoandaliwa na Wanachuo wenyewe chini ya Serikali ya Wanafunzi (ASO) ambapo jumla ya Shilingi 15,009,400/- kilikusanywa kwa ajili ya ujenzi wa vimbweta katika Kampasi ya Bagamoyo.