ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

PROF.MDOE (WyEST) ATAKA VYUO VYA UALIMU VIJIENDESHE

25 Feb, 2022
PROF.MDOE (WyEST) ATAKA VYUO VYA UALIMU VIJIENDESHE

Wito umetolewa kwa Wajumbe wa Bodi za Vyuo vya Ualimu nchini kwa kusaidiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha kwamba, Vyuo vya Ualimu nchini vinaweza kujiendesha ili kuongeza tija ufanisi katika uendeshaji wake.

Katika kufikia azma hiyo, wajumbe wa Bodi hizo wameaswa kuwa wabunifu na kutumia muda wao kufikiri namna mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, Vyuo hivyo vinaweza kujiendesha ikiwemo kutoa ushauri wa uanzishaji na uendelezaji wa miradi yenye tija.

Hayo yamesemwa Februari 14, 2022 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe alipokuwa akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi za Vyuo vya Ualimu nchini yaliyoendeshwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu nchini (ADEM) Bagamoyo Mkoani Pwani ambapo amewasisitiza kufuata Sheria, Kanuni, Sera za elimu pamoja na miongozo mbalimbali inayotolewa wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao.

Profesa Mdoe amesema, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji katika Vyuo vya Ualimu nchini kwa lengo la kuwapata Walimu wenye vigezo stahiki kwa mahitaji ya sasa na baadaye.

"Dhima ya Vyuo vya ualimu nchini ni kuandaa Walimu mahiri na wanaotosheleza mahitaji katika shule za awali, msingi na Sekondari. Kutokana na dhima hiyo, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji katika Vyuo vyote vya ualimu nchini" Amesema Profesa Mdoe

Ameendelea kwa kusema kuwa, baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itafanya ufuatiliaji wa karibu kwa kila Chuo cha ualimu ili kuona kama kila Bodi ya Chuo husika inatekeleza wajibu wake na kisha kutoa tathimini kuona tija iliyoongezeka katika utendaji kazi wa Bodi hizo pamoja na Chuo husika.

Vilevile Profesa Mdoe amezitaka Bodi hizo kuwa kiungo muhimu kati ya Chuo na Wizara lakini pia kuwa kiungo na jamii lengo ni kuimarisha ushirikishwaji wa wadau katika kuchangia maendeleo ya Chuo na kuisaidia Wizara ya Elimu katika kutekeleza majukumu yake.