ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

NAIBU KATIBU MKUU MyEST AFURAHIA MAFUNZO YA UONGOZI NA USIMAMIZI WA ELIMU YANAYOTOLEWA NA ADEM

15 Apr, 2023
NAIBU KATIBU MKUU MyEST AFURAHIA MAFUNZO YA UONGOZI NA USIMAMIZI WA ELIMU YANAYOTOLEWA NA ADEM

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia elimumsingi Dkt. Franklin Jasson Rwezimula leo Aprili 14 Aprili 2023 amefanya ziara ya kawaida kutembelea ofisi za Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu-ADEM Kampasi kuu Bagamoyo yenye lengo la kujionea shughuli zinazofanywa na ADEM.

Akiwa ADEM Bagamoyo Dkt. Rwezimula amepata fursa ya kuona miundombinu inayotumika katika ufundishaji na Ujifunzaji na machapisho mbalimbali kuhusu Uongozi na Usimamizi wa Elimu yaliyotolewa na Wakala na kuzungumza na Menejimenti na Watumishi.

ADkt. Rwezimula amesema lengo la ziara hiyo ni kuifahamu ADEM na kuona shughuli zinazofanywa na ADEM ambapo ametumia fursa hiyo kuipongeza Menejimenti ya ADEM kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yao unaopelekea ufikiwaji wa malengo waliyojiwekea.

“Nimeona mna mipango mingi mizuri mliyojiwekea, endeleeni nayo, ongezeni ubunifu katika namna ya utekelezaji wa majukumu ili kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, mitaala yenu izingatie ubunifu hii itawasaidia kuwa bora siku zote. Amesema Dkt. Rwezimula

Aidha Dkt Rwezimula amesisitiza ADEM kufanya ‘tracer study’ kufuatilia wanafunzi waliosoma ADEM kama wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi kulingana na elimu waliyoipata ADEM kwani itasaidia kujitathmini na kuboresha utoaji huduma.

Nae Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Siston Masanja Mgullah akielezea utekelezaji wa shughuli za Wakala kwa Naibu Katibu Mkuu Dkt. Rwezimula amesema ADEM imeendelea na utoaji wa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ya Uongozi, Usimamizi na Uthibiti Ubora wa Elimu, kufanya tafiti na kutoa machapisho mbalimbali na kutanabaisha kuwa nchi mbalimbali za Afrika zimekuja ADEM kujifunza namna ya kuanzisha taasisi ya Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa elimu ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Msumbiji na Afrika Kusini.

Dkt. Masanja pia ametumia fursa hiyo kuishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Mashirika ya Kimataifa kama vile UNICEF na World Bank kupitia miradi mbalimbali ya elimu kwa namna wanavyounga mkono utekelezaji wa shughuli za ADEM.

Katika ziara hiyo, Dkt. Rwezimula aliambatana na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Sebastian Innosh.