ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

MTENDAJI MKUU ADEM ASISITIZA UMUHIMU WA MAAFISA ELIMU KATA NCHINI KUJENGEWA UWEZO KUHUSU USIMAMIZI WA SHUGHULI ZA ELIMU

03 Jul, 2025
MTENDAJI MKUU ADEM ASISITIZA UMUHIMU WA MAAFISA ELIMU KATA NCHINI KUJENGEWA UWEZO KUHUSU USIMAMIZI WA SHUGHULI ZA ELIMU

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid J. Maulid, ameeleza Maafisa Elimu Kata wanawajibika kusimamia shughuli za elimu kwenye ngazi ya Kata, hivyo ni muhimu Maafisa hao kujengewa uwezo kuhusu usimamizi fanisi wa shughuli za elimu ili kuchagiza maendeleo ya sekta ya elimu katika ngazi ya Kata. 
Kauli hiyo aliitolewa 02 Julai, 2025 wakati akifungua mafunzo ya Utawala Bora katika Elimu kwa Maafisa Elimu Kata 343 kutoka mikoa ya Mbeya na Lindi na yanafanyika ADEM Bagamoyo.
Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha Maafisa Elimu Kata kusimamia kwa ufanisi shughuli za elimu katika ngazi ya kata, ili kuhakikisha ubora wa elimu unaimarika kuanzia ngazi ya jamii.
“Tumewapatia walimu wakuu wote nchini mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule ili waweze kusimamia ufundishaji na ujifunzaji shuleni, lakini Afisa Elimu Kata anatakiwa kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli za ufundishaji na ujifunzaji shuleni na ili kufanikisha hilo, mafunzo haya ya Utawala Bora wa Elimu yanatolewa kwenu ili yasaidie kwenda kufanya usimamamizi thabiti wa shughuli za elimu kwenye Kata mnazozisimamia”. Amesema Dkt. Maulid
Dkt. Maulid ameongeza kuwa, Maafisa Elimu Kata wanaoshiriki mafunzo hayo wana jukumu la kuhakikisha mafunzo watakayopatiwa yanaleta tija ili kuhakikisha thamani ya fedha zilizotumika kuendesha mafunzo haya inaonekana. Aidha, amewataka Maafisa Elimu Kata hao kwenda kuyatekeleza yale watakayojifunza kwa ufanisi. 
“Tunatarajia kuona matokeo chanya kuanzia ngazi ya shule hadi kata, kwa kusimamia ipasavyo yale mtakayojifunza katika mafunzo, ambapo ndiyo yatakuwa dira ya ufanisi katika usimamizi wa elimu”. amesisitiza Dkt. Maulid.
Nae mratibu wa mafunzo ya muda mfupi Bw. Huruma Mwenga, ameeleza kuwa washiriki wa mafunzo hayo watajengewa uwezo kuhusu uongozi, usimamizi na utawala katika elimu; utawala bora katika elimu; uandaaji wa mpango wa jumla wa maendeleo ya elimu katika ngazi ya serikali za mitaa; ufuatiliaji na usimamizi wa shule; usimamizi wa ujenzi wa miundombinu ya shule; ukaguzi wa ndani na ushirikishwaji wa jamii na utatuzi wa malalamiko katika sekta ya elimu.
Mafunzo ya Utawala Bora wa Elimu kwa Maafisa Elimu Kata wa Mkoa wa Mbeya na Lindi yanafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 02 - 04 Julai, 2025 kwa ufadhili wa mradi wa BOOST chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.