ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

MAFUNZO YA UONGOZI NA USIMAMIZI WA ELIMU YALENGE KUIMARISHA UTOAJI ELIMU BORA NCHINI: PROF. MKENDA

17 Feb, 2023
MAFUNZO YA UONGOZI NA USIMAMIZI WA ELIMU YALENGE KUIMARISHA UTOAJI ELIMU BORA NCHINI: PROF. MKENDA

Hayo yamesemwa leo Februari 17, 2023 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda alipotembelea Wakala na kujionea namna ambavyo Wakala unatekeleza majukumu yake ya kuendesha mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu nchini.

Prof. Mkenda amesema ni vema ADEM kuongeza uzito katika mafunzo ya maadili kwa Walimu  kwani wao ndio wasimamizi wa malezi, Ustawi wa Wanafunzi na maadili ya wanafunzi wawapo Shuleni,

“Elimu yetu inachukua masaa mengi ya mtoto kuwa darasani, hili linaumiza sana wanafunzi na kudunisha ustawi wao kama Watoto, pia masuala ya ukatili wa kijinsia yameongezeka shuleni, na kuporomoka kwa maadili ya Watoto shuleni. ADEM kama taasisi inayotoa mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa elimu, ione namna ya kufundisha walimu masuala ya malezi bora ya wanafunzi wawapo shuleni, maadili na kuimarisha ustawi wa wanafunzi shuleni” Amesema Prof. Mkenda.  

Ameongeza kuwa, Serikali imefanya maboresho makubwa katika sekta ya elimu nchini kwa kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, miundombinu imeongezwa Shuleni lakini bado mahitaji ni makubwa, ADEM iwafundishe walimu na viongozi wa elimu masuala ya utafutaji wa rasilimali na ushirikishwaji wa jamii katika uboreshaji wa miundombinu ya elimu, ili wakasimamie vema uboreshaji wa miundombinu ya elimu katika shule na maeneo wanayosimamia.  

“Suala lingine ambalo ni muhimu ADEM kuwafundisha walimu ni maadili katika usimamizi wa mitihani kwani kumekua na ukiukwaji wa maadili katika usimamizi wa mitihani nchini hali inayoweza kupelekea kutokua na ushindani halali wa kitaaluma baina ya wanafunzi. ADEM hakikisheni mnawafundisha walimu kuwa wasimamizi wazuri wa mitihani ili tujenge Taifa imara lenye wataalamu mahsusi waliopimwa na kufaulu kihalali hivyo kuinua kiwango chetu cha taaluma kama nchi. Amesema Prof. Mkenda.

Nae Mtendaji Mkuu ADEM, Dkt. Siston Masanja Mgullah amewasilisha utekelezaji wa majukumu ya Wakala mbele ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda ambapo amesema katika kipindi cha mwaka 2022/2023 ADEM imefanikiwa kudahili walimu 2,36 katika kozi za DEMA na DSQA, kuandaa Kitabu cha Kiongozi cha Mwalimu Mkuu, kuandaa Mwongozo wa Utawala Bora kwa Viongozi wa Serikali za Mitaa Pamoja na kuanza maandalizi ya ujenzi wa jengo la mihadhara katika Kampasi ya Bagamoyo lenye uwezo wa kuchukua Walimu 1000.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amefanya ziara ya kawaida kutembelea Wakala wa Maendeleo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu-ADEM ili kuona utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Wakala ambapo amefurahishwa na namna Wakala unavyotekeleza majukumu yake na kuahidi kuendelea kuboresha miundo mbinu ya Wakala ili kuimarisha utoaji wa mafunzo yanayotolewa na Wakala.