ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA ADEM:

30 Oct, 2022
KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA ADEM:

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imepongeza ADEM kwa namna inavyotekeleza shughuli zake hususani Utoaji wa Mafunzo ya Muda mrefu na Muda mfupi ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo akizungumza wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ADEM Oktoba 29, 2022 kuona utekelezaji wa shughuli za Wakala.

"Sisi kama wabunge tumefarijika sana, kuja hapa kumefanya tujue umuhimu wa Taasisi hii tumejifunza mengi hapa, tumepata uelewa wa kutosha na kama wajumbe wa kamati tumeongeza wigo wa uelewa ambao utatufanya kwenda kuishauri Serikali nini cha kufanya kuhusiana na Taasisi hii" Amesema Mhe. Nyongo

Kamati hiyo pia imepongeza upekee wa mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu yanayotolewa na Wakala kuwaandaa viongozi katika Sekta ya Elimu huku wakisisitiza kuwa Kiongozi bora na imara ndiye anayeweza kuleta mabadiliko chanya.

“Kamati hii inaunga mkono kwa Asilimia mia moja ADEM kuanzisha na kuendesha mafunzo ya Shahada ya Uthibiti Ubora wa Elimu kwani kama tulivyojionea wote katika taarifa ya Mtendaji Mkuu wa ADEM Shahada hiyo ni ya muhimu na itawaongezea umahiri Viongozi wa Elimu watakaofika ADEM kupatiwa mafunzo hayo katika Uthibiti Ubora wa masuala ya Elimu” Ameongeza Mhe. Nyongo

Nae Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Juma Kipanga ameishukuru Kamati hiyo kwa kutembelea ADEM na kujionea shughuli zinazotekelezwa na Wakala kwani ADEM ni Taasisi pekee chini ya Wizara hiyo inayoendesha mafunzo ya Uongozi kwa Viongozi wa Elimu nchini

Akizungumza mbele ya kamati hiyo, Kamishna wa Elimu nchini, Dkt Lyabwene Mtahabwa amesisitiza kuwa ili kufikia mafanikio chanya ya elimu ni lazima kuwaandaa Viongozi mahiri watakaosimamia Ubora katika utoaji wa Elimu nchini

"Ukiona Taasisi imejikita katika kuwajengea uwezo Viongozi hapo ndio pa kuongeza nguvu zetu, kwani kiongozi aliyepatiwa mafunzo ya Uongozi amepata uelewa wa namna ya kutekeleza majukumu yake kwa Ufanisi na kufikia malengo ya Taasisi anayoisimamia awe ni Mwalimu Mkuu, Afisa Elimu Kata, Afisa Elimu nk hivyo mafunzo yanayotolewa ADEM kuwajengea uwezo wakuu wa taasisi za Elimu ni ya muhimu sana katika kuimarisha Ubora wa Elimu nchini" Amesisitiza Dkt Mutahabwa.

Aidha, Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt Siston Masanja Mgullah akizungumza mbele ya Kamati hiyo ameiomba Kamati kuishauri Serikali pamoja na Wizara zinazohusika kuwasaidia Walimu wanaoomba kujiunga na ADEM ili kupata mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa elimu wanaokumbana na changamoto za kukosa ruhusa kutoka kwa waajiri wao pamoja na kukosa ufadhili wa malipo ya ada.

Kamati ya huduma na Maendeleo ya jamii ikiwa ADEM pia ilipata fursa ya kuzungumza na walimu takribani mia tano wa mwaka wa kwanza na wa pili wanaosoma Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu na Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule katika Kampasi ya Bagamoyo na kusikiliza changamoto zao hasa kunyimwa ruhusa na waajiri wao kwenda kujiendeleza kimasomo na Kamati kuahidi kuishauri Serikali changamoto hizo zipatiwe ufumbuzi.