DKT. AKWILAPO AZINDUA BARAZA LA WAFANYAKAZI LA ADEM: ASISITIZA MSHIKAMANO NA USHIRIKIANO

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri Dkt. Leonard Akwilapo ameongoza uzinduzi wa Baraza jipya la Wafanyakazi, ukionesha umuhimu wa mshikamano na ushirikiano kati ya uongozi na wafanyakazi wa Wakala. Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 15 Februari 2025, Mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Akwilapo amesema, Baraza hilo linaundwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2003 likiwa na kazi ya kutoa ushauri kwenye masuala yote yanayohusu watumishi mahala pa kazi.
Ameongeza kuwa, “Baraza hili ni msingi wa mafanikio yetu ya pamoja. Linatoa fursa kwa kila mfanyakazi kushirikisha mawazo yake kwa maendeleo ya taasisi na ustawi wa jamii ya ADEM”.
Hafla hiyo imehudhuriwa na wajumbe 32, wakiwemo wawakilishi wa idara ya Taaluma na Utawala, vyama vya wafanyakazi kama RAAWU na CWT, pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya Wakala.
Aidha, Mtendaji Mkuu Dkt. Maulid J. Maulid ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo amesisitiza kuwa Baraza hilo litafanya kazi kwa weledi kama wawakilishi wa watumishi wengine wa Wakala kwa kuwa mstari wa mbele katika kudadavua na kutoa mawazo chanya kwenye hoja mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye vikao vya Baraza la Wafanyakazi.
Dkt. Maulid ameongeza kuwa, “tuwe huru kutoa hoja na sisi kama Menejimenti tutazipokea na kuzifanyia kazi kwa haraka na kutoa mrejesho, tushirikiane kufanya kazi kwa bidii kwa kuhakikisha kwamba tunaongeza ubunifu katika utendaji wetu ili tuendane na maboresho makubwa yaliyofanyika katika Sekta ya elimu hasa maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na Mitaala iliyoboreshwa”.
Aidha, wawakilishi kutoka RAAWU na CWT walioshiriki hafla hiyo wamepongeza hatua ya kuanzishwa kwa baraza hilo na kusema kuwa Baraza hilo litasaidia kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha changamoto zinatatuliwa kwa haraka na kwamba ni jukwaa muhimu la kuimarisha mahusiano kazini.
Bw. Alphonce Mbassa mjumbe kutoka CWT amesisitiza na kuwataka wajumbe wa Baraza hilo kusikiliza changamoto za wafanyakazi na kuziwasilisha kwenye uongozi ili zitafutiwe ufumbuzi. "Nyie ni sauti ya wafanyakazi, hakikisheni masuala yao yanasikilizwa na mshirikiane na uongozi kuzitatua kwa wakati ili mahala pa kazi pawe ni mahali bora kutekeleza majukumu kwa kila mtumishi" alisema.
Baraza hilo linatarajiwa kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha mshikamano, mawasiliano, na utendaji kazi bora ndani ya Wakala hasa katika wakati huu ambapo Wakala unaunga jitihada za Serikali za maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na Mitaala iliyoboreshwa kwa kuimarisha usimamizi wa elimu ya Amali nchini.