ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

ADEM YATOA MAFUNZO KWA WAJUMBE 450 WA BODI 35 ZA VYUO VYA UALIMU NCHINI

01 Mar, 2022
ADEM YATOA MAFUNZO KWA WAJUMBE 450 WA BODI 35 ZA VYUO VYA UALIMU NCHINI

Wajumbe wa Bodi za Vyuo vya Ualimu wapatao 450 kutoka katika Vyuo vya Ualimu 35 vya Serikali wamepatiwa mafunzo Maalum ya Uongozi Fanisi wa Vyuo hivyo ADEM Bagamoyo kwa muda siku 7 yakiwa na lengo la kuwajengea Uwezo Wajumbe hao katika Usimamizi wa Vyuo vya Ualimu nchini ili kufikia malengo ya uboreshaji wa Sekta ya elimu nchini.

Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi Februari 8, 2022 ADEM Bagamoyo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo ambaye amesema Dhamira ya Wizara ni kuhakikisha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji yanaboreshwa kwa kuongeza miundombinu ya utoaji elimu pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa elimu katika ngazi mbali mbali kwa kuhakikisha inawapatia mafunzo kazini ya mara kwa mara ili kuwaongezea umahiri.

"Dhima ya Vyuo vya Ualimu nchini ni kuandaa Walimu mahiri na wanaotosheleza katika ngazi zote, hivyo wajumbe wa Bodi mna  dhima kubwa katika kuhakikisha dhamira hii inafikiwa kupitia wajibu wenu wa kushauri na kusimamia Vyuo vyenu" Amesema Prof. Nombo.

Nae Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Siston Masanja Mgullah akizungumza katika Ufunguzi wa mafunzo hayo amesema katika uendeshaji wa mafunzo hayo ADEM imezingatia mahitaji ya sasa ya Bodi za Vyuo vya Ualimu na yamelenga kuwaongezea umahiri Wajumbe wa Bodi hizo katika Usimamizi mahiri wa Vyuo vya Ualimu

"ADEM tumejipanga kuwawezesha Wajumbe hawa wa Bodi za Vyuo vya Ualimu juu ya Uongozi na Usimamizi mahiri wa Vyuo ambapo watajifunza juu ya Muundo na Majukumu ya Bodi ya Ushauri, Uandaaji mpango Mkakati wa Chuo, Utafutaji na Usimamizi wa Rasilimali za Chuo, Usimamizi w Sheria, Kanuni na Sera zinazohusu Elimu pamoja na Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji kazi wa Menejimenti za Vyuo vya Ualimu" Amesema Dkt. Masanja

Mafunzo kwa Bodi za Vyuo vya Ualimu yamelenga kuwajengea uwezo Wajumbe wa Bodi za Vyuo vya Ualimu nchini katika masuala ya Usimamizi wa Vyuo hivyo ambapo Wajumbe takribani 450 wanapatiwa mafunzo hayo kwa muda wa siku 7.