ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

ADEM YASAINI MKATABA WA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO NA TAASISI YA VVOB-EDUCATION FOR DEVELOPMENT YA NCHINI UBELGIJI KUIMARISHA UONGOZI NA USIMAMIZI WA ELIMU KWA VIONGOZI WA ELIMU NCHINI

29 Aug, 2025
ADEM YASAINI MKATABA WA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO NA TAASISI YA VVOB-EDUCATION FOR DEVELOPMENT YA NCHINI UBELGIJI KUIMARISHA UONGOZI NA USIMAMIZI WA ELIMU KWA VIONGOZI WA ELIMU NCHINI


WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu - ADEM umesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano - MoU na Shirika la Elimu lisilo la Kiserikali kutoka nchini Ubelgiji liitwalo VVOB-Education for Development kwa lengo la kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu nchini.

Akizungumza leo (Agosti 19, 2025) katika hafla ya utiaji saini uliofanyika katika Ofisi za ADEM, Bagamoyo, Mkurugenzi wa Sheria kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wakili Innocent Mgeta, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, alisema kupitia ushirikiano huo, ADEM itawajengea uwezo wakuu wa shule za Sekondari wapatao 12,000.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu - ADEM, Dkt. Maulid Maulid, amesema ushirikiano huo utasaidia serikali kufikia malengo yake kwa haraka kupitia mageuzi ya sera ya Elimu iliyoifanya.

Amesema kuwa taasisi yao inatarajia kunufaika kupitia ushirikiano huo katika masuala ya ujuzi wa TEHAMA na kuimarisha miundombinu ya TEHAMA ya Wakala.

“Ushirikiano huu ni hatua ya kihistoria katika jitihada zetu za kitaifa za kuimarisha uongozi wa shule kwa kuwajengea uwezo viongozi wa shule za sekondari kuhusu uongozi na usimamizi fanisi wa shule.
“Tunajivunia kushirikiana na VVOB na wadau wengine kuhakikisha kila mwanafunzi nchini anapata maarifa katika Taasisi ya Elimu anayongozwa na viongozi wa shule walio na uwezo, weledi na maono.” Amesema Dkt. Maulid.

Nae Mkurugenzi wa fedha – VVOB, Koenraad Van Den Steeln amesema VVOB imelenga kuwajengea uwezo viongozi wa shule za sekondari nchini,ambapo utawasaidia kuendesha shule hizo vizuri kuendana na mabadiliko ya sera ya Elimu.
“Tunasikia Fahari na furaha kubwa kushirikiana na ADEM na tuna imani kwamba kwa pamoja, tutajenga mfumo thabiti na imara wa uongozi nausimamizi wa elimu, mfumo unaolenga ufanisi wa elimu kwa kila mwanafunzi.” Amesisitiza