ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

ADEM WAADHIMISHA SIKU YA MWANAMKE

25 Feb, 2022
ADEM WAADHIMISHA SIKU YA MWANAMKE

 

Wanachuo wanawake takribani 350 wa ADEM ambao pia ni Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari nchini, wamejengewa uwezo juu ya masuala mbali mbali ya Kiafya, kijinsia, kijamii, kiuchumi na kitaaluma katika kongamano la   maadhimisho ya siku ya Mwanamke lililofanyika ADEM Bagamoyo Januari 23, 2022.

Katika maadhimisho hayo ambayo mgeni rasmi alikuwa ni Mtaalamu wa Afya kutoka Wizara ya Afya Dkt. Katanta Simwanza ambaye amewajengea uwezo Wanachuo hao Wanawake juu ya masuala ya Afya ya akili, mahusiano na malezi huku akisisitiza wanachuo hao kujitambua ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kama wanachuo na walimu

kuwasisitiza kuwa kujitambua ni suala muhimu kama Mwalimu anayetegemewa na Serikali na Wazazi kuwa mlezi wa Watoto wetu Shuleni, ni lazima ujitambue wewe ni nani ili utekeleze majukumu yako kwa ufanisi”. Amesema Dkt Katanta

Mtendaji Mkuu – ADEM, Dkt. Siston Masanja Mgullah, akizungumza katika kongamano hilo amesema ni vyema Wanawake watambue umuhimu wa mafunzo ya ziada wanayopewa nje ya mafunzo ya darasani kwani yatawasaidia katika kukuza taaluma zao na kufahamu mambo kwa upana zaidi.

“Katika kila mafunzo unayopatiwa ukiwa ADEM, ni lazima ujiulize yamekusaidia kupata uzoefu zaidi, elimu zaidi na ufahamu zaidi? Hilo ndio lengo la ADEM, kukujengea uwezo zaidi wa kielimu, kuyafahamu mambo kwa uhalisia na upana zaidi na kukuongzea uzoefu katika masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kielimu” Amesema Dkt. Masanja

Kongamano hilo pia lilipambwa na wawezeshaji wa mada mbalimbali akiwa ni Pamoja na Bi. Zaida Mgalla ambaye ni Mkurugenzi wa UWEZO Tanzania aliyefundisha juu ya Mbinu rahisi za ufundishaji wa kusoma, kuandika na kuhesabu (K.K.K) kwa kutumia programu ya Jifunze akishirikaiana na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii (Organisation for Community Development - OCODE) waliofanya uwasilishaji wa shughuli wanazotekeleza ili kuboresha elimu hasa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Nae Katibu wa CWT Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Shaaban Iddy Tessua ametumia Kongamano hilo kutoa elimu kwa Wanachuo hao Wanawake juu ya kutambua Wajibu na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Haki na wajibu wa Mtumishi Mwalimu awapo masomoni na atakaporudi kazini baada ya kumaliza masomo

Kadhalika, Mtaalam wa masuala ya Ujasiriamali Bw. Kelvin Kibenje amezungumzia masuala ya Ujasiriamali kwa Wanawake hasa biashara ya uwekezaji wa pesa kutazama fursa na kuzifanyia kazi, pia Walimu wanawake kubuni vyanzo vya mapato bila kuathiri shughuli za mwajiri huku Bi. Linda Mshana ambaye ni Mkurugenzi wa Masoko kutoka SELF Microfinance iliyo chini ya Wizara ya Fedha, akizungumzia huduma za mikopo nafuu kwa Watumishi hususani Walimu.

Kongamano hilo la Mwanamke la Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu ADEM, limekwenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Elimu ya Umoja wa Mataifa na kuratibiwa na Champion Chanzige Organisation ambao wameahidi kuendelea na uratibu wa kongamano hilo kila Mwaka.