ADEM, CAMFED YAWASILISHA MAPENDEKEZO YA MABORESHO YA MUUNDO WA KAMATI NA BODI ZA SHULE NCHINI

🗓️23 Septemba, 2025
📍Dodoma
ADEM kwa kushirikiana na CAMFED Tanzania wamefanya uwasilishaji wa maoni na mapendekezo ya kuthibitisha wazo la kitaalamu kuhusu maboresho ya Muundo wa Bodi na Kamati za Shule lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi hizo mbili kwa lengo la kuishauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhusu maboresho kwenye Muundo wa Bodi na Kamati za Shule. Uwasilishaji huo umefanyika katika Ofisi za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia i Dodoma
Akimwakilisha Kamishna wa Elimu nchini Dkt. Lyabwene Mutahabwa aliyekuwa Mgeni Rasmi, Patrick Leana, Afisa mwandamizi kutoka WyEST amesema mapendekezo ya maboresho ya Muundo wa Bodi na Kamati za Shule yaliyowasilishwa kwa wadau mbalimbali wa Elimu na kisha kuwasilishwa kwenye Menejimenti ya Wizara ya Elimu kupitia warsha hiyo, limekuja katika wakati mwafaka ambao Wizara ya Elimu inatekeleza maboresho makubwa katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2014 toleo la 2023 ambayo inapigia chapuo uongozi bora wa shule kama chachu ya mafanikio ya utoaji elimu bora katika ngazi ya shule.
“ADEM ina wajibu wa kuishauri Wizara kuhusu namna bora ya kuimarisha uongozi na usimamizi wa shule, inatia moyo tunapoona mnafanya kazi hiyo kwa weledi kama yalivyo matarajio ya Wizara. Kikao kazi hiki cha leo kinathibitisha hilo kuwa mnaifanya kazi hiyo kwa weledi, ufanisi na ubunifu mkubwa ndio maana mnashirikiana pia na taasisi zingine za Serikali na zisizo za Serikali kuhakikisha uongozi na usimamizi wa elimu unaimarishwa”. Amesema Bw. Patrick Leana.
Nae Mtendaji Mkuu - ADEM Dkt. Maulid J. Maulid akizungumza katika kikao kazi hicho cha uwasilishaji wa mapendekezo hayo amesema ADEM itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kuhakikisha inaishauri Wizara zinazosimamia elimu katika eneo la uongozi na usimamizi fanisi wa shule kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu ndani na nje ya Nchi ili kuboresha elimu yetu.
“ADEM inashirikiana na CAMFED katika kipindi cha mwaka mmoja kuimarisha uongozi na usimamizi wa shule kupitia kuimarisha mifumo ya uongozi wa shule hususani Bodi na Kamati za Shule na katika kutekeleza hilo tumepitia Muundo wa wa Bodi na Kamati za Shule na kupendekeza maboresho katika Muundo huo ili kuzifanya Bodi na Kamati za Shule zitekeleze majukumu yake kwa ufanisi kwa kuzingatia usawa wa kijinsi na ujumuishi ili zitoe maamuzi sahihi yenye tija kwa ustawi wa elimu yetu nchini” Amesema Dkt. Maulid.
Kikao kazi hicho kimefanyika katika Ofisi za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia jijini Dodoma tarehe 23 Septemba, 2025 na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu, Maafisa kutoka Ofisi ya Kamishna wa elimu pamoja na Menejimenti ya ADEM na CAMFED.