ADEM Logo

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu

ADEM, CAMFED WAFANYA MAPITIO YA MUUNDO WA KAMATI NA BODI ZA SHULE KUSAIDIA KUIMARISHA USIMAMIZI WA SHULE NCHINI

01 Sep, 2025
ADEM, CAMFED WAFANYA MAPITIO YA MUUNDO WA KAMATI NA BODI ZA SHULE KUSAIDIA KUIMARISHA USIMAMIZI WA SHULE NCHINI

29 Agosti, 2025
📍Dar es Salaam

ADEM kwa kushirikiana na CAMFED Tanzania wameendesha Warsha ya kupokea maoni na mapendekezo ya kuthibitisha wazo la kitaalamu kuhusu maboresho ya Muundo wa Bodi na Kamati za Shule lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi hizo mbili kwa lengo la kuishauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhusu maboresho kwenye Muundo wa Bodi na Kamati za Shule. 

Akimwakilisha Kamishna wa Elimu nchini Dkt. Lyabwene Mutahabwa aliyekuwa Mgeni Rasmi, Fredy Nyandaro, Afisa mwandamizi kutoka WyEST amesema wazo hilo lililowasilishwa kwa wadau mbalimbali wa Elimu kupitia warsha hiyo, limekuja katika wakati mwafaka ambao Wizara ya Elimu inatekeleza maboresho makubwa katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2014 toleo la 2023 anbayo inapigia chapuo uongozi bora wa shule kama chachu ya mafanikio ya utoaji elimu bora katika ngazi ya shule.

Nae Mtendaji Mkuu - ADEM Dkt. Maulid J. Maulid akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo amesema ADEM itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kuhakikisha inaishauri Wizara zinazosimamia elimu katika eneo la uongozi na usimamizi fanisi wa shule kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu ndani na nje ya Nchi ili kuboresha elimu yetu.

Warsha hiyo imefanyika leo tarehe 29 Agosti, 2025 jijini Dar es Salaam ikiongozwa na ADEM pamoja na CAMFED na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu ikiwa ni pamoja na Asasi za Kiraia zinazoshughulika na masuala ya Elimu, Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri pamoja na Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule